Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa yeye, kama walivyo Watanzania wengine, hana wasiwasi na
uwezo wa wajumbe wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba
kuifanya kazi hiyo vizuri na kwa ufanisi mkubwa.
Aidha,
Rais Kikwete amewataka wajumbe wa Tume hiyo kuwa huru kabisa katika
kuifanya kazi yao bila kuruhusu kuingiliwa na mtu yoyote.
Rais
Kikwete amesema hayo jioni ya leo, Jumanne, Mei 15, 2012 wakati
alipote mbelea Ofisi za Tume hiyo zilizoko Mtaa wa Ohio, mjini Dar es
Salaam, akakagua ofisi hizo na kuzungumza kwa ufupi na wajumbe wa Tume
hiyo ambayo iko chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Sinde Warioba na
Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhan.
Akizungumza
na wajumbe wa Tume hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa ana uhakika kuwa
wajumbe wa Tume hiyo watatimiza matarajio ya Watanzania katika kuifanya
vizuri kazi ya Kukusanya na Kuratibu maoni ya wananchi kuhusu Katiba
mpya.
“Nimefurahi
kusikia kuwa mumeianza kazi yetu vizuri. Nawaombeni muwe huru kabisa
katika kuifanya kazi yetu. Na kwa ubora wa sifa za wajumbe, binafsi,
kama walivyo Watanzania wengine sina wasiwasi juu ya uwezo wenu kuifanya
kazi hii vizuri,” Rais Kikwete amewaambia wajumbe waTume hiyo na
kuongeza:
“Kilichobakia kwetu ni lini milango itafunguliwa ili tuanze kutoa maoni yetu …. huo ndiyo mchango wetu katika mchakato huu.”
Mapema
akimkaribisha Mheshimiwa Rais, Jaji Warioba amesema kuwa Tume hiyo
ilianza kazi kama ilivyotakiwa kisheria Mei Mosi mwaka huu na kuwa kazi
ambazo zimefanyika mpaka sasa ni wajumbe kujielimisha kuhusu Sheria
yenyewe ya Katiba na kuorodhesha Hadidu za Rejea za Tume.
“Mheshimiwa
Rais tumetumia wiki hii ya kwanza ya kazi yetu kujielimisha kuhusu
Sheria yenyewe iliyounda Tume hii na pia tumeorodhesha Hadidu za Rejea
za Tume. Tumeanza pia maandalizi kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa umma
na baada ya hapo tutatengeneza ratiba ya kazi yetu,” amesema Jaji
Warioba na kuongeza:
“Tumeanza
kuona kuwa kazi hii itakuwa siyo rahisi na muda ni mfupi lakini
itafanyika. Tunakushukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ya uteuzi wa
Tume na imani ambayo umeionyesha kwetu kwa kutuchagua kutumikia katika
Tume hii.”
Rais
pia amejulishwa kwa kazi ya kuajiri watumishi wa Tume hiyo imeanza na
mpaka sasa wameajiriwa watumishi 29 kati ya 173 wanaotakiwa kufanya kazi
kwenye tume hiyo ambayo itaifanya kazi ya Kukusanya na Kuratibu maoni
kwa miezi 18 kuanzia Mei Mosi mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment