Halmashauri
ya Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi imegundua udanganyifu na
ubadhirifu mkubwa wa dawa unaofikia karibu Sh. milioni 100.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri ya
Kilwa Adoh Mapunda, alifichua kuwa udanganyifu huo unafanywa na baadhi
ya watumishi wa halmashauri wanaopokea dawa hizo kutoka Bohari ya Dawa
(MSD ) na kuziingiza katika zahanati hewa ambazo hata ujenzi wake
haujakamilika.
Ripoti hizo zinakuja wiki chache baada ya
Bunge kuchachamaa kutaka ubadhirifu wa fedha na mali za umma ukomeshwe
kwenye halmashauri na serikali kuu, hatua iliyosababisha baadhi ya
Mawaziri kuwajibishwa wakiwemo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Mapunda , alikifahamisha kikao cha Baraza
la Madiwani kilichofanyika hivi karibuni juu ya ubadhirifu huo na
kuongeza kuwa kwa miaka mitatu watumishi hao wameiba madawa yenye
thamani ya Sh. milioni 83.2 kwa kuyaingiza kwenye zahanati hewa.
Alisema kiasi hicho cha dawa zilihujumiwa
katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2010 kwa kusingizia kuwa
kinapelekwa katika zahanati nane ambazo ujenzi wake haujakamilika.
Alizitaja zahanati hewa mbele ya baraza
hilo kuwa ni Mitole, Hoteli Tatu, Kiranjeranje, Kisongo, Mchakama,
Nangurukuru pamoja na vituo vya Mikole na Kimbalambala.
Kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi wa
hesabu wa ndani iliyosomwa na mkurugenzi huyo alibainisha kuwa ukaguzi
umeibua kuwepo vituo vinane ambavyo ujenzi wake haujakamilika lakini
vimepatiwa usajili na kila kimoja hutengewa gawio la Sh milioni 7.3 kwa
ajili ya dawa. Mkaguzi wa ndani alifanya uchunguzi wake katika vituo 51
vya kutolea huduma za matibabu.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa katika
ukaguzi wa ndani ambaye yeye mwenyewe alimpatia jukumu la kufuatilia
hujuma hizo mara baada ya kuhamishiwa kwenye halmashauri hiyo,
imegundulika kuwa, vituo viwili kati ya hivyo vinane vilipewa gawio la
dawa za thamani ya Sh.milioni 14.7 kila kimoja na vilivyosalia vilipata
gawio la dawa za thamani ya Sh. milioni 7.3 kila kimoja.
Kutokana na takwimu zilizotolewa na
Mkurugenzi wa Halmashauri inaonyesha kwamba madawa ambayo yalipelekwa
kwenye zahanati hizo nane hewa yana thamani ya Sh. milioni 83.2 na
haijafahamika mgao huo wa madawa ulikuwa ukipelekwa wapi.
Mapunda aliliambia baraza hilo la madiwani
kuwa hali hiyo ni hujuma kubwa kwa serikali ambapo imeisababishia
halmashauri kukumbwa na tatizo la kupelekewa dawa zisizohitajika, kwa
maana kwamba kiasi hicho cha madawa kingeweza kupelekwa katika sehemu
nyingine nchini.
Halmashauri ya wilaya ya Kilwa ina jumla ya zahanati 43, Vituo vya Afya vitano na hospitali mbili.
Baraza la madiwani ambalo lilimpongeza
mkurugenzi huyo kwa kufanikisha kugundua ufisadi huo na lilipitisha
azimio la kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, watumishi wote
wanaotuhumiwa kufanya udanganyifu wa kupokea dawa kutoka Bohari ya Dawa
na kuziingiza katika zahanati hewa.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake,
Mahadhi Nangoma, Diwani wa Lihimalyao, alisema hoja hizo zinapaswa
kufanyiwa kazi ipasavyo ili iwe fundisho kwa watendaji wenye tabia ya
kutumia vibaya madaraka yao.
Vitendo hivyo vya ubadhirifu vilifanyika
wakati ambapo wakurugenzi zaidi ya wanne walikuwa wamefanyakazi katika
Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kabla ya Mkurugenzi wa sasa kuhamishiwa
katika halmashauri hiyo na kugundua ubadhirifu huo.
SOURCE:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment