Test Footer

Latest Post

Shibuda kuwania urais akiwa Chadema

Written By mahamoud on Tuesday, May 15, 2012 | 3:07 PM



BAADA ya mwaka 2005 kuwania urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kubwagwa katika hatua za awali, Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda, kwa mara nyingine ametangaza kuwania nafasi hiyo kwa tiketi ya Chadema mwaka 2015.

Shibuda alitangaza azma yake hiyo juzi mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kwenye semina iliyofanyika Dodoma katika ukumbi wa Nec ya CCM iliyojadili hali ya utawala bora nchini iliyotolewa na taasisi inayotathmini utawala bora Afrika (APRM).

Shibuda ni mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo anayewakilisha vyama vya upinzani.

"Nakupa pole, kazi ya urais ni ngumu sana, bila shaka utakumbuka kuwa nami nilitaka kuwa mbadala wako, hata hivyo naamini utakuwa meneja wangu wa kampeni za urais mwaka 2015," alisema Shibuda.

Huku wajumbe wa NEC wakishangalia, Rais Kikwete alimwuliza: "unataka urais kupitia chama gani?" Shibuda akajibu kwa kujiamini: "Kupitia Chadema, huku niliko sasa”.

Kauli ya Shibuda imekuja wakati kukiwa na minong'ono ya baadhi ya wanasiasa wazito ndani ya chama hicho kutaka kuwania nafasi hiyo.

Wanasiasa wanaotajwa kutaka kwa udi na uvumba kuwania nafasi hiyo kupitia Chadema, ni Mwenyekiti wa Chama hicho, Mbunge wa Hai Freeman Mbowe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa ambaye aliwania mwaka 2010.

Huku akishangiliwa na wajumbe wa NEC Shibuda alisema kwa kuwa mwaka 2005 aliomba ridhaa ya CCM kugombea urais akakosa nafasi hiyo alimwomba Rais Kikwete awe mpiga debe wake na kuamini kuwa kwa kazi nzuri aliyofanya nchini kwa kipindi cha miaka aliyokaa madarakani, akimpigia debe bila shaka atafanikiwa.

Kikwete akamwuliza anataka ampigie debe kupitia chama gani? Shibuda akajibu “kupitia Chadema,” wajumbe wa NEC wakamshangilia kwa nderemo na vigelegele.

Shibuda pia alizungumzia nafasi ya CCM katika siasa ya Tanzania, na kusisitiza kuwa hivi sasa hakuna mbadala wa CCM katika kuongoza nchi.

Alisisitiza kuwa CCM imejijenga kimfumo kuanzia ngazi ya juu mpaka mashinani, jambo ambalo linarahisisha utoaji haki kuanzia chini mpaka juu.

Mbunge huyo, alisisitiza kuwa tatizo ndani ya CCM ni baadhi ya viongozi kuwa wabinafsi ambao aliwafananisha na kunguru wasiofugika, kwa kutofuata miiko na maadili ya chama na badala yake kuwa sehemu ya watu wanaoharibu chama hicho.

Hata hivyo, alisema pamoja na yote, bado nafasi ya CCM kuendelea kuongoza Dola ni kubwa, kwani mpaka sasa vyama vya siasa vya upinzani, bado havijawa na uwezo wa kutekeleza chochote zaidi ya CCM.
Chanzo:habari leo

UDOM sasa kufundisha kwa MTANDAO!

Katika kuhakikisha kuwa tunakwenda na kasi ya teknologia inayoenda kwa kasi duniani, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) sasa kimeanza rasmi kufundisha kwa kutumia mtandao na kuhakikisha
kila mhadhiri, anafundisha madenti wengi kwa wakati mmoja.
Hilo liliwekwa wazi juzi na Balozi Juma Mwapachu, alipokuwa akizungumza na wahadhiri wa Udom katika ufunguzi wa mafunzo ya ufundishaji kwa njia ya teknolojia hiyo.
Mwapacha ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, alisema wingi wa wanafunzi katika chuo hicho kikubwa kwa sasa hauendani na idadi ya wahadhiri waliopo na kwamba bila ya  kuwa na mbinu mbadala za kuwafundisha, wanafunzi wataachwa nyuma.
 “Udom sio chuo cha kawaida katika nchi za Afrika Mashariki, lakini pia niseme kuwa siyo vyuo vingi hapa duniani vimeweza kupata bahati ya kukua kwa kasi kubwa ndani ya miaka minne kama Udom, kwa hiyo ukuaji wa chuo hiki lazima uwe wa kisasa na unaokwenda na sayansi na teknolijia,” alisema
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Udom, Prof Idris Kikula, alisema chuo kilikuwa kinakabiliwa na tatizo katika ufundishaji, hatua iliyoulazimisha uongozi kubuni mkakati huo.Kikula alisema hatua ya sasa ni ya kuwajengea uwezo wahadhiri, ili waweze kufanyakazi zao kwa ufanisi mkubwa zaidi.


Mbunge atimua mbio Mahakamani!

Katika hali ambayo iliwafanya watu waangue kicheko, Mbunge wa Kilwa Kusini, Suleiman Said Bungara (CUF), mwishoni mwa wiki alitoa kali ya mwaka kwa kutimua mbio kwa pilato (mahakamani) baada ya Jaji Fatuma Masenga wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, kuthibitisha ushindi wake.
Ushindi wa mbunge huyo ulikuwa ukipingwa mahakamani na mjumbe wa Halmashauri Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ramadhani Madabida.
Mara baada ya hukumu hiyo kumalizika kusomwa, mbunge huyo alitoka nje ya ukumbi wa mahakama akiwa ameweka mikono kichwani mithili ya mtu aliyefiwa.
Akiwa kama vile haamini kilichotokea mahakamani, alipofika barabarani ghafla alitimua mbio na maelfu ya wananchama wa CUF walimfuata kwa nyuma, kisha kumzingira na kumbeba juu.
Huku wakiimbia nyimbo za kuikejeli CCM, wafuasi hao wa CUF walizunguka mji mzima wa Kilwa wakiimba na kubeba kitu mithili ya jeneza lililovishwa bendera za CCM.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua saa 5, Jaji Masenga alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, umeshindwa kuthitibisha madai ya mlalamikaji.
Katika kesi hiyo, Madabida alidai mbunge huyo wakati wa kampeni mwaka 2010, alitumia kauli za ukabila kwamba mlalamikaji si mkazi wa Kilwa.

mtoto mwenye jinsia mbili kichwani

MTOTO mwenye maumbile ya ajabu akiwa na jinsia mbili za kiume na moja ya kike amezaliwa Aprili 25 mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma mjini Songea. Mtoto huyo ambaye bado yupo hai chini ya uangalizi maalum amezaliwa akiwa na hitilafu katika maumbile yake ikiwa ni pamoja na kuzaliwa na nusu ya ubongo ambayo imetokana na hitilafu kwenye mfumo wa kichwa hadi uti wa mgongo.
Muuguzi wa zamu katika wodi ya wazazi katika hospitali ya mkoa ambako mtoto huyo anaangaliwa Agness Mwinuka amesema mtoto huyo ambaye amezaliwa na uzito wa kilo moja na gramu 900 amezaliwa akiwa na jinsia mbili za kiume na jinsia moja ya kike.

Picha hii inamuonesha mtoto aliyezaliwa katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma akiwa na maumbile ya ajabu yakiwemo jinsia mbili za kiume  na jinsia moja ya kike ambazo zipo juu ya kichwa chake ambacho pia kimeumbwa kwa nusu ya ubongo hali ambayo inahatarisha maisha ya mtoto huyo aliyezaliwa akiwa na uzito wa karibu kilo mbili baada ya kutimiza miezi tisa.
“Jinsia moja ya kiume ipo kama kawaida isipokuwa jinsia moja ya kiume ipo kichwani karibu na kisogo na jinsia ya kike ipo utosini, mtoto huyu tangu azaliwe juzi hadi sasa hana uwezo wa kunyonya wala kula kitu chochote, uchunguzi wa kitabibu bado unaendelea’’,alisisitiza.
Mama mzazi wa mtoto huyo Situmahi Mwinuka(32) mkazi wa Msamala mjini Songea anasema huyu ni mtoto wake wa nne kuzaliwa na kwamba watoto wake wengine watatu hawajawahi kupata hitilafu yeyote katika mwili.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma Dk.Mathayo Chanangula akielezea hali ya mtoto huyo alisema mtoto anakabiliwa na tatizo ambalo kitaalam ni hitilafu kwenye mfumo unaoanzia kichwani hadi kwenye uti wa mgongo ambao umesababisha mtoto huyo kuzaliwa na nusu ya ubongo.
Kulingana na daktari huyo hitilafu hiyo imesababisha mifumo ya mwili kuwa na dosari ambapo kuna sehemu mbili za kiume moja ikiwa kichwani na kwamba mtoto anapolia sehemu ya kiume ya kichwani inasimama na kusisitiza kuwa maisha ya mtoto huyo ni mafupi kutokana na mifumo ya mwili wake kutokamilika licha ya kwamba mtoto amezaliwa na miezi tisa.
“Katika nchi zilizoendelea madaktari bingwa na wenye vifaa vya kisasa wanaweza kuokoa maisha ya mtoto huyo,hata kama mtoto huyo anaokolewa atakabiliwa na tatizo kubwa la ulemavu wa akiri kwa kuwa ubongo alionao ni nusu tu ya ubongo unaotakiwa kwa binadamu kamili’’,alisisitiza.
Dk. Chanangula anabainisha kuwa mama mjamzito anaweza kujifungua mtoto mwenye maumbile ya ajabu iwapo atakosa madini aina ya folic acid ambayo alisisitiza ni muhimu kwa mama mjamzito kunywa madini hayo miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito wake.
“Mama anaweza kujifungua mtoto mwenye maumbile ya ajabu iwapo katika miezi mitatu ya mwanzo katika ujauzito wake atatumia dawa aina ya flagile, dawa za minyoo, tetesakline na baadhi ya dawa za malaria kama vile SP ambayo anaruhisiwa kunywa baada ya wiki 28 na ALU ambayo hairuhusiwi kabisa kutumika kwa mjamzito kwa ujumla ni marufuku mama mjamzito kunywa dawa bila kumuona daktari’’,alisisitiza.
Katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma hili ni tukio la kwanza la aina yake mtoto kuzaliwa akiwa na hitilafu kubwa katika mifumo ya mwili wake.
Habari hii imeandikwa na Albano Midelo

JK: SINA WASI WASI NA UWEZO WA WAJUME WA TUME YA KUKUSANYA NA KURATIBU MAONI YA KATIBA MPYA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa yeye, kama walivyo Watanzania wengine, hana wasiwasi na uwezo wa wajumbe wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba kuifanya kazi hiyo vizuri na kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, Rais Kikwete amewataka wajumbe wa Tume hiyo kuwa huru kabisa katika kuifanya kazi yao bila kuruhusu kuingiliwa na mtu yoyote.
Rais Kikwete amesema hayo jioni ya leo, Jumanne, Mei 15, 2012 wakati alipote    mbelea Ofisi za Tume hiyo zilizoko Mtaa wa Ohio, mjini Dar es Salaam, akakagua ofisi hizo na kuzungumza kwa ufupi na wajumbe wa Tume hiyo ambayo iko chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhan.
Akizungumza na wajumbe wa Tume hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa ana uhakika kuwa wajumbe wa Tume hiyo watatimiza matarajio ya Watanzania katika kuifanya vizuri kazi ya Kukusanya na Kuratibu maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya.
“Nimefurahi kusikia kuwa mumeianza kazi yetu vizuri. Nawaombeni muwe huru kabisa katika kuifanya kazi yetu. Na kwa ubora wa sifa za wajumbe, binafsi, kama walivyo Watanzania wengine sina wasiwasi juu ya uwezo wenu kuifanya kazi hii vizuri,” Rais Kikwete amewaambia wajumbe waTume hiyo na kuongeza:
“Kilichobakia kwetu ni lini milango itafunguliwa ili tuanze kutoa maoni yetu …. huo ndiyo mchango wetu katika mchakato huu.”
Mapema akimkaribisha Mheshimiwa Rais, Jaji Warioba amesema kuwa Tume hiyo ilianza kazi kama ilivyotakiwa kisheria Mei Mosi mwaka huu na kuwa kazi ambazo zimefanyika mpaka sasa ni wajumbe kujielimisha kuhusu Sheria yenyewe ya Katiba na kuorodhesha Hadidu za Rejea za Tume.
“Mheshimiwa Rais tumetumia wiki hii ya kwanza ya kazi yetu kujielimisha kuhusu Sheria yenyewe iliyounda Tume hii na pia tumeorodhesha Hadidu za Rejea za Tume. Tumeanza pia maandalizi kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa umma na baada ya hapo tutatengeneza ratiba ya kazi yetu,” amesema Jaji Warioba na kuongeza:
“Tumeanza kuona kuwa kazi hii itakuwa siyo rahisi na muda ni mfupi lakini itafanyika. Tunakushukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ya uteuzi wa Tume na imani ambayo umeionyesha kwetu kwa kutuchagua kutumikia katika Tume hii.”
 
Rais pia amejulishwa kwa kazi ya kuajiri watumishi wa Tume hiyo imeanza na mpaka sasa wameajiriwa watumishi 29 kati ya 173 wanaotakiwa kufanya kazi kwenye tume hiyo ambayo itaifanya kazi ya Kukusanya na Kuratibu maoni kwa miezi 18 kuanzia Mei Mosi mwaka huu.

Halmashauri yagundua ubadhirifu dawa za mil.100/-

Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi imegundua udanganyifu na ubadhirifu mkubwa wa dawa unaofikia karibu Sh. milioni 100.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri ya Kilwa Adoh Mapunda, alifichua kuwa udanganyifu huo unafanywa na baadhi ya watumishi wa halmashauri wanaopokea dawa hizo kutoka Bohari ya Dawa (MSD ) na kuziingiza katika zahanati hewa ambazo hata ujenzi wake haujakamilika.
Ripoti hizo zinakuja wiki chache baada ya Bunge kuchachamaa kutaka ubadhirifu wa fedha na mali za umma ukomeshwe kwenye halmashauri na serikali kuu, hatua iliyosababisha baadhi ya Mawaziri kuwajibishwa wakiwemo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Mapunda , alikifahamisha kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika hivi karibuni juu ya ubadhirifu huo na kuongeza kuwa kwa miaka mitatu watumishi hao wameiba madawa yenye thamani ya Sh. milioni 83.2 kwa kuyaingiza kwenye zahanati hewa.
Alisema kiasi hicho cha dawa zilihujumiwa katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2010 kwa kusingizia kuwa kinapelekwa katika zahanati nane ambazo ujenzi wake haujakamilika.
Alizitaja zahanati hewa mbele ya baraza hilo kuwa ni Mitole, Hoteli Tatu, Kiranjeranje, Kisongo, Mchakama, Nangurukuru pamoja na vituo vya Mikole na Kimbalambala.
Kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi wa hesabu wa ndani iliyosomwa na mkurugenzi huyo alibainisha kuwa ukaguzi umeibua kuwepo vituo vinane ambavyo ujenzi wake haujakamilika lakini vimepatiwa usajili na kila kimoja hutengewa gawio la Sh milioni 7.3 kwa ajili ya dawa. Mkaguzi wa ndani alifanya uchunguzi wake katika vituo 51 vya kutolea huduma za matibabu.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa katika ukaguzi wa ndani ambaye yeye mwenyewe alimpatia jukumu la kufuatilia hujuma hizo mara baada ya kuhamishiwa kwenye halmashauri hiyo, imegundulika kuwa, vituo viwili kati ya hivyo vinane vilipewa gawio la dawa za thamani ya Sh.milioni 14.7 kila kimoja na vilivyosalia vilipata gawio la dawa za thamani ya Sh. milioni 7.3 kila kimoja.
Kutokana na takwimu zilizotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri inaonyesha kwamba madawa ambayo yalipelekwa kwenye zahanati hizo nane hewa yana thamani ya Sh. milioni 83.2 na haijafahamika mgao huo wa madawa ulikuwa ukipelekwa wapi.
Mapunda aliliambia baraza hilo la madiwani kuwa hali hiyo ni hujuma kubwa kwa serikali ambapo imeisababishia halmashauri kukumbwa na tatizo la kupelekewa dawa zisizohitajika, kwa maana kwamba kiasi hicho cha madawa kingeweza kupelekwa katika sehemu nyingine nchini.
Halmashauri ya wilaya ya Kilwa ina jumla ya zahanati 43, Vituo vya Afya vitano na hospitali mbili.
Baraza la madiwani ambalo lilimpongeza mkurugenzi huyo kwa kufanikisha kugundua ufisadi huo na lilipitisha azimio la kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, watumishi wote wanaotuhumiwa kufanya udanganyifu wa kupokea dawa kutoka Bohari ya Dawa na kuziingiza katika zahanati hewa.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake, Mahadhi Nangoma, Diwani wa Lihimalyao, alisema hoja hizo zinapaswa kufanyiwa kazi ipasavyo ili iwe fundisho kwa watendaji wenye tabia ya kutumia vibaya madaraka yao.
Vitendo hivyo vya ubadhirifu vilifanyika wakati ambapo wakurugenzi zaidi ya wanne walikuwa wamefanyakazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kabla ya Mkurugenzi wa sasa kuhamishiwa katika halmashauri hiyo na kugundua ubadhirifu huo.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. KILWA FORUMS - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website
Proudly powered by Blogger