Test Footer

Latest Post

Aliye kuwa Rais wa Egypt Hosni Mubarak ahukumiwa kifungo cha maisha

Written By mahamoud on Saturday, June 2, 2012 | 10:38 AM


Egypt's Muslim Brotherhood (MB) presidential hopeful Mohamed Morsi says the life sentence for former dictator Hosni Mubarak is a “farce,” calling for mass protests against the verdict.


On Saturday, Morsi called for mass protests in the capital Cairo's Liberation Square to protest at Mubarak's verdict, saying the former dictator must face retrial that should provide necessary evidence for a just punishment.

In a final verdict hearing in a Cairo court on Saturday, the ex-dictator as well as former Interior Minister Habib al-Adli were sentenced to life imprisonment for the killing of around 900 protesters during the country’s popular uprising that ended his three-decade rule.


The court also dropped charges against six other security officials, who were brought to trial for the killing of the protesters.

The verdict sparked fierce clashes between the families of the victims and security officials inside the court.

Angry spectators called the court illegitimate and demanded the execution of Mubarak.

Meanwhile, Mubarak’s last premier, who faces Morsi in presidential runoff on June 16-17, said the life sentence against the former dictator "must be accepted."

Hotuba Rais Kikwete 02/06/2012

Ndugu Wananchi,

Kama ilivyo ada, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa
kutujaalia uhai na kutuwezesha kumaliza mwezi Mei salama. Kwa kutumia
utaratibu wetu wa kuzungumza kwa njia hii kila mwisho wa mwezi, leo
nitazungumzia mambo matatu.

Mkutano wa G-8
Jambo la kwanza, ni suala la usalama wa chakula na lishe. Duniani,
inakadiriwa kuwa kuna watu milioni 925 wanaokabiliwa na njaa na lishe
duni. Kati ya hao Afrika ina watu milioni 239 ambao ni karibu theluthi
moja ya watu wote wenye tatizo la njaa na lishe duni kote duniani.
Nchi za Afrika zenye tatizo la njaa kiasi cha kuhitaji msaada wa
chakula kutoka nje ni 27. Kati ya hizo 11 zina matatizo makubwa zaidi.
Tanzania siyo miongoni mwa nchi hizo, hata hivyo bado hatujafikia
kiwango cha kujitosheleza kabisa. Hivi sasa tumefikia asilimia 95 na
kila mwaka yapo maeneo nchini yanayopata msaada wa chakula kutoka
Serikalini.

Mwaka 2009, katika mkutano wao wa L’Aquila, Italia, viongozi wa nchi
nane tajiri kuliko zote duniani waliamua kuchukua hatua ya kuzisaidia
nchi zinazoendelea duniani kukabiliana na tatizo la njaa na lishe
duni. Katika mkutano ule waliahidi kutoa dola za Marekani bilioni 22
kwa ajili hiyo. Tanzania tunategemea kupata dola milioni 22.9.

Katika mkutano wa nchi hizo maarufu kwa jina la G-8 uliofanyika Camp
David, Marekani tarehe 19 Mei, 2012, pamoja na mambo mengine
walizungumzia suala la usalama wa chakula na lishe barani Afrika. Nia
yao ni kuchangia katika juhudi zinazofanywa na mataifa ya Afrika zenye
shabaha ya kutokomeza matatizo hayo. Tofauti na walivyofanya L’Aquila,
safari hii waliamua kuchangia katika utekelezaji wa mipango na progamu
za kuendeleza kilimo katika nchi za Afrika hasa zile zinazolenga
kujenga usalama wa chakula na lishe.

Aidha, waliamua kuwa wataanza na nchi tatu na kuendelea kuziongeza
kila baada ya muda fulani, badala ya kuanza na nchi zote mara moja.
Hoja yao kubwa ni kwamba, wanataka kukusanya nguvu zao kwa nchi hizo
chache ili kufanya kazi ambayo itakuwa na matokeo yanayoonekana katika
kutokomeza njaa na kuboresha lishe. Hawakupenda kusambaza nguvu zao
kwa nchi nyingi na kuishia kutokufanya kazi ya maana.


Ndugu wananchi;
Bahati nzuri katika programu na mipango ya nchi iliyokubaliwa kwa
awamu ya kwanza ni Tanzania, Ethiopia na Ghana. Na, jambo la
kufurahisha zaidi ni kwamba mpango wetu wa kuendeleza kilimo katika
ukanda wa Kusini mwa Tanzania ulichukuliwa kuwa ni wa mfano. Maoni
hayo ya nchi za G-8 ndiyo maoni ya WEF, Sekretariat ya NEPAD na Umoja
wa Afrika, wote wameona kuwa mpango wetu unafaa kuenezwa barani Afrika
kama mkakati sahihi wa kuendeleza kilimo, kujitosheleza kwa chakula na
kupunguza umaskini.

Katika Bara la Afrika mkakati huo sasa unaitwa Grow Africa Partnership
na tayari nchi saba zimeshajiunga nao. Nchi hizo ni Tanzania,
Msumbiji, Kenya, Rwanda, Ethiopia, Ghana na Burkina Faso.
Katika mkutano wa Camp David, nchi za Marekani, Japani, Uingereza,
Ujerumani, Ufaransa na Urusi zimeahidi kuchangia nchi yetu katika
juhudi zetu za kuendeleza kilimo na hasa zile zenye lengo la
kujitosheleza kwa chakula na kuboresha lishe nchini. Ukichanganya na
ahadi iliyotolewa na Umoja wa Ulaya katika mkutano huo, kiasi cha dola
za Marekani milioni 897 zimeahidiwa kutolewa kwa nchi yetu kati ya
sasa na mwaka 2015.

Ndugu Wananchi;
Mwaka 2006 tulizindua Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo nchini
maarufu kwa kifupi kama ASDP. Kwa kirefu kwa lugha ya Kiingereza ni
the Agricultural Sector Development Programme. Programu hii ndiyo
mwanzo wa safari yetu ya uhakika ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini
Tanzania. Jambo la kwanza lililofanyika katika utayarishaji wa
Programu hii ni kutambua vikwazo vinavyozuia maendeleo ya kilimo
nchini na kupendekeza hatua za kuchukua za kuondosha vikwazo hivyo.

Mwaka 2008, katika tathmini iliyofanywa kwa ushirikiano wa Serikali na
Sekta Binafsi kwa uamuzi wa Baraza la Biashara Tanzania, ilidhihirika
kwamba sekta binafsi ambayo ni wadau muhimu, haijahusishwa vya kutosha
katika mikakati, mipango na programu za kuendeleza kilimo nchini. Kwa
pamoja ilikubaliwa kuwa kasoro hiyo iondolewe ili wadau wote
washirikishwe, yaani Serikali, wakulima wadogo, wakulima wakubwa na
sekta binafsi. Vilevile, sote tulikubaliana kutoa kipaumbele cha juu
kwa maendeleo ya kilimo. Kwa pamoja tuliafikiana kuwa mambo mengine
yanaweza kusubiri isipokuwa kilimo. Matokeo ya maelewano hayo ndiyo
yaliyozaa mkakati na kauli mbiu ya “Kilimo Kwanza”.

Ndugu Wananchi;
Tangu wakati huo, sekta binafsi nchini imekuwa inahusishwa na
kushirikishwa kwa karibu katika utekelezajiwa ASDP na kuendeleza
kilimo kwa jumla. Kwa upande mmoja sekta binafsi imekuwa inahusishwa
katika upatikanaji wa zana na pembejeo za kisasa za kilimo kwa
wakulima. Kwa ajili hiyo, wenzetu wa sekta binafsi wamekuwa
wanategemewa kuleta na kuuza matrekta, mitambo na vifaa mbalimbali vya
kilimo pamoja na mbegu, mbolea, dawa za kuua wadudu waharibifu wa
mazao na za kukinga na kutibu maradhi ya mimea na mifugo. Hali
kadhalika, wamekuwa wanajihusisha na ununuzi na usindikaji wa mazao ya
mkulima na kuongeza thamani. Tunataka tuachane na kuendelea kuuza nje
mazao ya kilimo kama malighafi na kununua bidhaa zilizotengenezwa na
mazao hayo.

Upande mwingine tuliwategemea wenzetu wa sekta binafsi washiriki
kulima mashamba makubwa. Wasiache kazi ya kilimo kufanywa na wakulima
wadogo peke yao ambao uwezo wao si mkubwa wa kukabili matatizo ya
kuongeza tija. Nafurahi kwamba wito wangu huo waliupokea vizuri na
baadhi yao wameshaanza kufanya hivyo.

Ndugu Wananchi;
Swali kubwa walilouliza ndugu zetu hao siku ile ya tarehe 2 – 3 Juni,
2009 pale Kunduchi Beach Hotel ni kuhusu upatikanaji wa ardhi.
Niliwaeleza kuwa upo utaratibu mzuri wa kuwapatia wakulima wakubwa
ardhi ya kilimo na ufugaji. Utaratibu wenyewe ni kwamba kila wilaya
imetakiwa kutenga ardhi kwa ajili ya wakulima wakubwa. Hilo
likishafanyika, taarifa hutolewa kwa Kituo cha Uwekezaji na kuingizwa
katika kitu kinachoitwa Benki ya Ardhi. Mwekezaji anapojitokeza,
kulingana na aina ya kilimo anachotaka kujihusisha nacho, hugawiwa
ardhi hiyo. Ardhi hiyo ni ile ambayo siyo inayotumiwa na wakulima
wadogo. Katu hawanyang’anywi ardhi wakulima wadogo ili kuwapa wakulima
wakubwa. Hiyo siyo sera wala madhumuni na malengo ya ASDP au Kilimo
Kwanza.
Nalifafanua hili kuondoa hofu iliyokuwepo na upotoshaji uliokuwa
unafanywa makusudi wa kuhusisha wakulima wakubwa na uporaji wa ardhi.
Siyo makusudio yake hata kidogo.

Ndugu Wananchi;
Mwaka 2010 tukapanua wigo wa ushiriki wa sekta binafsi kwa kuihusisha
sekta binafsi ya kutoka nje ya nchi. Mwaka huo pia, tukaamua kuipa
sekta binafsi lengo maalum la kutekeleza nalo ni kushiriki katika
kilimo cha kuhakikisha kuwa nchi yetu inajitosheleza kwa chakula na
kupata ziada kubwa ya kuuza nje, kwa majirani zetu na kwingineko.
Shabaha yetu hasa ilikuwa ni kujitosheleza kwa vyakula vikuu vya
mahindi, mchele na sukari.

Aidha, tuliamua pia kuwa, kwa kuanzia tuelekeze nguvu zetu kwenye
mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Iringa na Morogoro kwa vile mikoa hiyo
ndiyo ghala la chakula la nchi yetu. Kwa vile mikoa hiyo ipo ukanda wa
kusini ndio maana ikaja kuitwa Southern Agriculture Growth Corridor of
Tanzania au SAGCOT. Tumeamua tukusanye nguvu za Serikali, wakulima,
sekta binafsi na washirika wetu wa maendeleo kuwekeza katika
kuendeleza kilimo katika mikoa hiyo.

Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mpango wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa SAGCOT una
shabaha kuu mbili: Kwanza kabisa mpango unalenga kuboresha kilimo cha
wakulima wadogo ili kitoke kuwa duni na cha kujikimu na kuwa cha
kisasa na kibiashara. Chini ya mpango huu wakulima wadogo watasaidiwa
na kuwezeshwa kupata na kutumia zana na pembejeo za kisasa za kilimo.
Pia watawezeshwa kupata mikopo kwa ajili ya kilimo na masoko ya
uhakika na yenye bei nzuri kwa mazao yao. Vile vile, huduma muhimu
zitaimarishwa. Hapa tunazungumzia maafisa ugani na miundombinu ya
umwagiliaji, barabara, umeme, maji safi na teknolojia ya habari na
mawasiliano.

Pili, kwa pale inapowezekana kwa maana ya upatikanaji wa ardhi na aina
ya mazao, kuihusisha sekta binafsi katika kilimo. Tayari utekelezaji
wa mpango wa SAGCOT umeanza. Kamati ya Utendaji imeshaundwa na
Sekretariati yake imeshateuliwa. Aidha, Mfuko wa Kuchochea Uwekezaji
umeshaanzishwa na unaendelea kuchangiwa fedha.

Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa malengo ya SAGCOT kwa kilimo cha mpunga na kuongeza
uzalishaji wa sukari yameanza kutekelezwa. Matayarisho yanaendelea kwa
kilimo cha mahindi na mazao mengine.

Mpango huu utakapofanikiwa utakuwa na manufaa makubwa. Nchi yetu
itajitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada kubwa ya kuuza nje.
Inakadiriwa kuwa mapato yatokanayo na kilimo katika ukanda huu
yatafikia dola bilioni 1.2 kwa mwaka, watu 420,000 watapata ajira na
watu 2,000,000 wataondokana na umaskini uliokithiri.

Uwekezaji wake ni mkubwa na kwamba kiasi cha dola bilioni 3.4
kinahitajika kwa kipindi cha miaka 20. Kwa ushirikiano uliopo baina ya
Serikali, sekta binafsi na wabia wetu wa maendeleo wakiwemo wa nchi za
G-8, hayo yote yanawezekana.

Ndugu Wananchi;
Tukijitosheleza kwa chakula na kwa maana pana ya chakula chenye lishe
bora tutakuwa tumefanikiwa kupata ufumbuzi wa tatizo kubwa la ukosefu
wa lishe bora miongoni mwa wananchi wa Tanzania. Wanaoathirika sana na
tatizo hili ni kina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya
miaka mitano. Ukosefu wa lishe bora huchangia asilimia 20 ya vifo vya
kinamama wajawazito nchini na theluthi moja ya watoto wa umri wa chini
ya miaka mitano. Aidha, asilimia 42 ya watoto wa umri wa chini ya
miaka mitano wamedumaa na asilimia 16 wana uzito mdogo kulingana na
umri wao na asilimia 59 wana upungufu wa damu. Kwa kina mama
wajawazito asilimia 41 wana matatizo ya upungufu wa damu. Hali hii sio
nzuri hata kidogo lazima tuibadili na tunaweza kufanya hivyo. Tunao
mkakati wa kitaifa wa kuboresha lishe ambao kwa sehemu kubwa
utanufaika sana na kufanikiwa kwa mkakati wa kujitosheleza kwa
chakula.

Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
Ndugu Wananchi;
Jana tarehe 31 Mei, 2012 nilishiriki katika sherehe za ufunguzi wa
Mkutano wa 47 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na
Mkutano wa 38 wa Mfuko wa Maendeleo wa Afrika. Hii ni mara ya kwanza
katika historia ya Benki hii tangu ianzishwe mwaka 1964 kwa nchi yetu
kuwa mwenyeji wa mikutano hii inayofanyika kila mwaka. Ni heshima
kubwa sana kwa nchi yetu, nami kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote,
nimemshukuru sana Rais wa Benki hiyo, Dkt. Donald Kaberuka kwa ihsani
kubwa aliyoifanyia nchi yetu.

Kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu ni jambo lenye manufaa mengi
kwetu. Kwanza husaidia kuitangaza nchi yetu Barani Afrika na
kwingineko duniani. Pili, ni fursa nzuri ya kuzungumza na viongozi wa
Benki kuhusu mipango na miradi yetu ya maendeleo tunayohitaji msaada
kutoka Benki hiyo.

Na, tatu, ni fursa nzuri ya watu wetu kufanya biashara. Mkutano huu
umeshirikisha watu 2,500 ambao wametoka nje ya Tanzania na
wanajitegemea kwa kila kitu. Wenye hoteli, migahawa, vyombo vya
usafiri, huduma ya simu, internet na nyinginezo watakuwa wamefanya
biashara nzuri katika wiki nzima kabla ya tarehe 28 Mei mkutano
ulipoanza hadi 2 Juni, mkutano utakapofungwa. Ni kutokana na manufaa
kama haya, ndio maana huwa tunahangaika kuvutia mikutano mikubwa kuja
kufanyikia hapa nchini.

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa ndugu
zetu wa Arusha kwa kuwapokea vizuri na kuwakarimu vyema wageni wetu
hao. Nawaomba waendelee na moyo huo mpaka watakapoondoka wote. Naomba
kuwepo kwa mkutano huu kuwakumbushe umuhimu wa mji wenu kuwa tulivu.
Miaka miwili iliyopita isingekuwa rahisi kwa watu au shirika kubwa la
kimataifa kama Benki hii kuamua kufanya mkutano wake Arusha. Isitoshe
hata sisi wenyewe tusingeshawishika kuomba au kukubali maombi ya namna
hiyo. Lakini sasa imewezekana. Naomba kila mmoja wetu aweke azimio
moyoni mwake la kuhakikisha kuwa hali ile haijirudii tena. Nyota ya
Geneva ya Afrika lazima iendelee kuangaza. Yaliyopita si ndwele
tugange yajayo.

Watanzania Wenzangu;
Niruhusuni tena niwashukuru wenzetu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
kwa mchango mkubwa waliotoa na wanaoendelea kutoa kuchangia maendeleo
ya nchi yetu. Kwa miaka mingi Benki hii imekuwa inatupatia mikopo na
misaada muhimu kwa maendeleo ya sekta mbalimbali nchini pamoja na zile
za elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara, reli, umeme n.k.

Kwa msaada wa Benki hii tunajenga barabara ya Namanga – Arusha,
Minjingu – Singida, Namtumbo – Tunduru, Iringa – Dodoma, Mayamaya –
Babati, na Tunduru – Mangaka – Mtambaswala. Miaka ya nyuma pia
walituwezesha kujenga barabara ya Mutukula – Muhutwe. Aidha, hivi sasa
wanagharamia upembuzi yakinifu na usanifu wa reli mpya tunayotaka
kuijenga kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda na Burundi.

Matukio ya Uvunjifu wa Amani Zanzibar
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni matukio ya wiki
iliyopita huko kwenye Jiji la Zanzibar katika mkoa wa Mjini Magharibi,
Unguja. Kama tujuavyo sote kulitokea ghasia zilizochochewa na viongozi
wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu maarufu kwa jina la
Uamsho. Taasisi hii imeanzishwa kwa madhumuni ya kidini, lakini hivi
sasa viongozi wake wameamua kuyaacha madhumuni hayo na kubeba ajenda
za siasa.

Siku za nyuma, ndugu zetu hawa walikuwa wakitumia muda mwingi kuilaumu
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya kuundwa kwa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa lawama hizo sasa hazisikiki. Lakini, mara
tulipoanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, mihadhara yao imeelekezwa kupinga Muungano na
kuwakashifu viongozi waasisi wa Muungano na hata waliopo sasa.
Isitoshe wamekuwa wakipandikiza chuki dhidi ya ndugu zao wa kutoka
Tanzania Bara na wale wafuasi wa dini ya Kikristo.

Baya zaidi, katika uchochezi huo majengo na mali za Makanisa mawili
zilichomwa moto, maduka ya watu kuvunjwa na mali zao kuibiwa. Kwa
kweli vitendo hivi ni uhalifu ambao haukubaliki na wala hauvumiliki.
Naungana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kauli yake aliyoitoa jana katika
mkutano wake na waandishi wa habari ya kukemea vikali na kulaani
uhalifu huo.

Ndugu Wananchi;
Ni jambo la kusikitisha na kushangaza kwamba, wenzetu hawa wamefanya
uhalifu huo kwa hoja ya kupinga Muungano. Haiwezekani mtu anayepinga
Muungano, akaitetea hoja yake kwa kuchoma moto makanisa au kuvunja
maduka ya watu na kupora mali zao. Ukristo haukuingizwa Zanzibar na
Muungano, bali ulikuwepo karne kadhaa kabla ya Muungano na wala
haukutokea Tanzania Bara. Na kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais Ali
Mohamed Shein jana, ukweli ni kwamba, dini ya Kikristo kama ilivyo ya
Kiislamu imeenezwa Bara kutokea Zanzibar. Kanisa kuu la Anglikan
Zanzibar lilijengwa kuanzia mwaka 1873 na lile la Katoliki kuanzia
1893 ni miongoni mwa Makanisa makongwe kuliko mengi kama siyo yote kwa
upande wa Zanzibar na Bara.

Katika hotuba yake ya jana, Mheshimiwa Rais, Dkt. Ali Mohamed
Shein,pamoja na kueleza kwa ufasaha ukweli huu, pia alisisitiza suala
la haki na uhuru wa Kikatiba wa mtu kuchagua au kubadilisha dini au
imani yake. Katika kutumia uhuru huo, mtu hastahili kuingiliwa au
kulazimishwa na mtu yo yote. Hayo pia ndiyo matakwa ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kweli yanayofanywa na ndugu zetu
wa Uamsho ya kuchoma moto makanisa siyo sawa hata kidogo. Na,
wanapoyafanya kwa kisingizio cha Muungano ni jambo lisiloeleweka
kabisa na wala halina mantiki. Labda wenzetu wana lao jambo.

Ndugu Wananchi;
Jambo lingine la kushangaza zaidi ni kule kutokea vurugu na ghasia
hizi dhidi ya Muungano wakati ambapo Serikali imetoa fursa sasa kwa
watu kutoa maoni yao kwenye mjadala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kama tujuavyo sote, Tume ya Katiba imekwishaundwa na inajiandaa kupita
kote nchini kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba mpya waitakayo.
Kama mtu ana maoni yake kuhusu Muungano, hiyo ndiyo fursa ya kufanya
hivyo. Utaratibu mzuri umewekwa kwa ajili yetu sote, vurugu za nini?

Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Mimi sioni sababu ya msingi ya kusababisha kuvurugika kwa amani kwa
jambo ambalo limewekewa utaratibu muafaka wa kulishughulikia. Nawaomba
tutumie utaratibu mzuri uliowekwa badala ya kufanya mambo yanayoleta
mifarakano katika jamii na yanayosababisha uvunjifu wa amani na
yanaharibu sifa na sura ya Wazanzibari na Watanzania isivyostahili.

Ndugu zangu,
Haipendezi wala haifurahishi kwa Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya
raia wake. Lakini, kama hapana budi, Serikali lazima ifanye na
haitasita kufanya hivyo. Narudia kuwasihi viongozi na wafuasi wa
Jumuiya ya Uamsho kurejea kwenye madhumuni ya msingi ya jumuiya yao.
Wajiepushe na ajenda za kisiasa na kupandikiza chuki zitakazosababisha
mifarakano baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano na baina
ya Wakristo na Waislamu. Watanzania ni ndugu na wamekuwa wanaishi
pamoja kwa upendo na furaha licha ya tofauti zao za rangi, makabila,
dini na maeneo watokako. Kimeharibika kipi hata leo yatokee haya?
Aidha nawaomba wenye maoni kuhusu Muungano wetu, muundo wake na
uendeshaji wake watumie fursa ya mjadala wa Katiba kutoa maoni yao.
Huhitaji kufanya ghasia kutoa maoni yako!

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia fursa hii pia kuwapa pole wale wote walioathirika na
vurugu zilizotokea. Nawaomba wawe wastahamilivu, hiyo ndiyo mitihani
ya maisha. Serikali zetu mbili zitafanya kila lililo kwenye mamlaka
yake kuwahakikishia wananchi wote usalama wa maisha yao na wa mali
zao.

Nawapongeza vijana wetu wa Jeshi la Polisi kwa juhudi kubwa
waliyoifanya ya kudhibiti hali ambayo mwelekeo wake haukuwa mwema.
Nawaomba waendelee kuwa macho ili watu wasioitakia mema nchi yetu na
watu wake wasipate nafasi ya kutuvurugia amani na utulivu wetu.
Naamini tukidumisha utamaduni wetu wa kuheshimiana, kuvumiliana na
kuzungumza pale tunapotofautiana hakuna litakaloharibika. Haya shime
tufanye hayo.


Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.

Shibuda kuwania urais akiwa Chadema

Written By mahamoud on Tuesday, May 15, 2012 | 3:07 PM



BAADA ya mwaka 2005 kuwania urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kubwagwa katika hatua za awali, Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda, kwa mara nyingine ametangaza kuwania nafasi hiyo kwa tiketi ya Chadema mwaka 2015.

Shibuda alitangaza azma yake hiyo juzi mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kwenye semina iliyofanyika Dodoma katika ukumbi wa Nec ya CCM iliyojadili hali ya utawala bora nchini iliyotolewa na taasisi inayotathmini utawala bora Afrika (APRM).

Shibuda ni mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo anayewakilisha vyama vya upinzani.

"Nakupa pole, kazi ya urais ni ngumu sana, bila shaka utakumbuka kuwa nami nilitaka kuwa mbadala wako, hata hivyo naamini utakuwa meneja wangu wa kampeni za urais mwaka 2015," alisema Shibuda.

Huku wajumbe wa NEC wakishangalia, Rais Kikwete alimwuliza: "unataka urais kupitia chama gani?" Shibuda akajibu kwa kujiamini: "Kupitia Chadema, huku niliko sasa”.

Kauli ya Shibuda imekuja wakati kukiwa na minong'ono ya baadhi ya wanasiasa wazito ndani ya chama hicho kutaka kuwania nafasi hiyo.

Wanasiasa wanaotajwa kutaka kwa udi na uvumba kuwania nafasi hiyo kupitia Chadema, ni Mwenyekiti wa Chama hicho, Mbunge wa Hai Freeman Mbowe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa ambaye aliwania mwaka 2010.

Huku akishangiliwa na wajumbe wa NEC Shibuda alisema kwa kuwa mwaka 2005 aliomba ridhaa ya CCM kugombea urais akakosa nafasi hiyo alimwomba Rais Kikwete awe mpiga debe wake na kuamini kuwa kwa kazi nzuri aliyofanya nchini kwa kipindi cha miaka aliyokaa madarakani, akimpigia debe bila shaka atafanikiwa.

Kikwete akamwuliza anataka ampigie debe kupitia chama gani? Shibuda akajibu “kupitia Chadema,” wajumbe wa NEC wakamshangilia kwa nderemo na vigelegele.

Shibuda pia alizungumzia nafasi ya CCM katika siasa ya Tanzania, na kusisitiza kuwa hivi sasa hakuna mbadala wa CCM katika kuongoza nchi.

Alisisitiza kuwa CCM imejijenga kimfumo kuanzia ngazi ya juu mpaka mashinani, jambo ambalo linarahisisha utoaji haki kuanzia chini mpaka juu.

Mbunge huyo, alisisitiza kuwa tatizo ndani ya CCM ni baadhi ya viongozi kuwa wabinafsi ambao aliwafananisha na kunguru wasiofugika, kwa kutofuata miiko na maadili ya chama na badala yake kuwa sehemu ya watu wanaoharibu chama hicho.

Hata hivyo, alisema pamoja na yote, bado nafasi ya CCM kuendelea kuongoza Dola ni kubwa, kwani mpaka sasa vyama vya siasa vya upinzani, bado havijawa na uwezo wa kutekeleza chochote zaidi ya CCM.
Chanzo:habari leo

UDOM sasa kufundisha kwa MTANDAO!

Katika kuhakikisha kuwa tunakwenda na kasi ya teknologia inayoenda kwa kasi duniani, Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) sasa kimeanza rasmi kufundisha kwa kutumia mtandao na kuhakikisha
kila mhadhiri, anafundisha madenti wengi kwa wakati mmoja.
Hilo liliwekwa wazi juzi na Balozi Juma Mwapachu, alipokuwa akizungumza na wahadhiri wa Udom katika ufunguzi wa mafunzo ya ufundishaji kwa njia ya teknolojia hiyo.
Mwapacha ambaye pia ni Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, alisema wingi wa wanafunzi katika chuo hicho kikubwa kwa sasa hauendani na idadi ya wahadhiri waliopo na kwamba bila ya  kuwa na mbinu mbadala za kuwafundisha, wanafunzi wataachwa nyuma.
 “Udom sio chuo cha kawaida katika nchi za Afrika Mashariki, lakini pia niseme kuwa siyo vyuo vingi hapa duniani vimeweza kupata bahati ya kukua kwa kasi kubwa ndani ya miaka minne kama Udom, kwa hiyo ukuaji wa chuo hiki lazima uwe wa kisasa na unaokwenda na sayansi na teknolijia,” alisema
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Udom, Prof Idris Kikula, alisema chuo kilikuwa kinakabiliwa na tatizo katika ufundishaji, hatua iliyoulazimisha uongozi kubuni mkakati huo.Kikula alisema hatua ya sasa ni ya kuwajengea uwezo wahadhiri, ili waweze kufanyakazi zao kwa ufanisi mkubwa zaidi.


Mbunge atimua mbio Mahakamani!

Katika hali ambayo iliwafanya watu waangue kicheko, Mbunge wa Kilwa Kusini, Suleiman Said Bungara (CUF), mwishoni mwa wiki alitoa kali ya mwaka kwa kutimua mbio kwa pilato (mahakamani) baada ya Jaji Fatuma Masenga wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, kuthibitisha ushindi wake.
Ushindi wa mbunge huyo ulikuwa ukipingwa mahakamani na mjumbe wa Halmashauri Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ramadhani Madabida.
Mara baada ya hukumu hiyo kumalizika kusomwa, mbunge huyo alitoka nje ya ukumbi wa mahakama akiwa ameweka mikono kichwani mithili ya mtu aliyefiwa.
Akiwa kama vile haamini kilichotokea mahakamani, alipofika barabarani ghafla alitimua mbio na maelfu ya wananchama wa CUF walimfuata kwa nyuma, kisha kumzingira na kumbeba juu.
Huku wakiimbia nyimbo za kuikejeli CCM, wafuasi hao wa CUF walizunguka mji mzima wa Kilwa wakiimba na kubeba kitu mithili ya jeneza lililovishwa bendera za CCM.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua saa 5, Jaji Masenga alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, umeshindwa kuthitibisha madai ya mlalamikaji.
Katika kesi hiyo, Madabida alidai mbunge huyo wakati wa kampeni mwaka 2010, alitumia kauli za ukabila kwamba mlalamikaji si mkazi wa Kilwa.

mtoto mwenye jinsia mbili kichwani

MTOTO mwenye maumbile ya ajabu akiwa na jinsia mbili za kiume na moja ya kike amezaliwa Aprili 25 mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma mjini Songea. Mtoto huyo ambaye bado yupo hai chini ya uangalizi maalum amezaliwa akiwa na hitilafu katika maumbile yake ikiwa ni pamoja na kuzaliwa na nusu ya ubongo ambayo imetokana na hitilafu kwenye mfumo wa kichwa hadi uti wa mgongo.
Muuguzi wa zamu katika wodi ya wazazi katika hospitali ya mkoa ambako mtoto huyo anaangaliwa Agness Mwinuka amesema mtoto huyo ambaye amezaliwa na uzito wa kilo moja na gramu 900 amezaliwa akiwa na jinsia mbili za kiume na jinsia moja ya kike.

Picha hii inamuonesha mtoto aliyezaliwa katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma akiwa na maumbile ya ajabu yakiwemo jinsia mbili za kiume  na jinsia moja ya kike ambazo zipo juu ya kichwa chake ambacho pia kimeumbwa kwa nusu ya ubongo hali ambayo inahatarisha maisha ya mtoto huyo aliyezaliwa akiwa na uzito wa karibu kilo mbili baada ya kutimiza miezi tisa.
“Jinsia moja ya kiume ipo kama kawaida isipokuwa jinsia moja ya kiume ipo kichwani karibu na kisogo na jinsia ya kike ipo utosini, mtoto huyu tangu azaliwe juzi hadi sasa hana uwezo wa kunyonya wala kula kitu chochote, uchunguzi wa kitabibu bado unaendelea’’,alisisitiza.
Mama mzazi wa mtoto huyo Situmahi Mwinuka(32) mkazi wa Msamala mjini Songea anasema huyu ni mtoto wake wa nne kuzaliwa na kwamba watoto wake wengine watatu hawajawahi kupata hitilafu yeyote katika mwili.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma Dk.Mathayo Chanangula akielezea hali ya mtoto huyo alisema mtoto anakabiliwa na tatizo ambalo kitaalam ni hitilafu kwenye mfumo unaoanzia kichwani hadi kwenye uti wa mgongo ambao umesababisha mtoto huyo kuzaliwa na nusu ya ubongo.
Kulingana na daktari huyo hitilafu hiyo imesababisha mifumo ya mwili kuwa na dosari ambapo kuna sehemu mbili za kiume moja ikiwa kichwani na kwamba mtoto anapolia sehemu ya kiume ya kichwani inasimama na kusisitiza kuwa maisha ya mtoto huyo ni mafupi kutokana na mifumo ya mwili wake kutokamilika licha ya kwamba mtoto amezaliwa na miezi tisa.
“Katika nchi zilizoendelea madaktari bingwa na wenye vifaa vya kisasa wanaweza kuokoa maisha ya mtoto huyo,hata kama mtoto huyo anaokolewa atakabiliwa na tatizo kubwa la ulemavu wa akiri kwa kuwa ubongo alionao ni nusu tu ya ubongo unaotakiwa kwa binadamu kamili’’,alisisitiza.
Dk. Chanangula anabainisha kuwa mama mjamzito anaweza kujifungua mtoto mwenye maumbile ya ajabu iwapo atakosa madini aina ya folic acid ambayo alisisitiza ni muhimu kwa mama mjamzito kunywa madini hayo miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito wake.
“Mama anaweza kujifungua mtoto mwenye maumbile ya ajabu iwapo katika miezi mitatu ya mwanzo katika ujauzito wake atatumia dawa aina ya flagile, dawa za minyoo, tetesakline na baadhi ya dawa za malaria kama vile SP ambayo anaruhisiwa kunywa baada ya wiki 28 na ALU ambayo hairuhusiwi kabisa kutumika kwa mjamzito kwa ujumla ni marufuku mama mjamzito kunywa dawa bila kumuona daktari’’,alisisitiza.
Katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma hili ni tukio la kwanza la aina yake mtoto kuzaliwa akiwa na hitilafu kubwa katika mifumo ya mwili wake.
Habari hii imeandikwa na Albano Midelo

JK: SINA WASI WASI NA UWEZO WA WAJUME WA TUME YA KUKUSANYA NA KURATIBU MAONI YA KATIBA MPYA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa yeye, kama walivyo Watanzania wengine, hana wasiwasi na uwezo wa wajumbe wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba kuifanya kazi hiyo vizuri na kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, Rais Kikwete amewataka wajumbe wa Tume hiyo kuwa huru kabisa katika kuifanya kazi yao bila kuruhusu kuingiliwa na mtu yoyote.
Rais Kikwete amesema hayo jioni ya leo, Jumanne, Mei 15, 2012 wakati alipote    mbelea Ofisi za Tume hiyo zilizoko Mtaa wa Ohio, mjini Dar es Salaam, akakagua ofisi hizo na kuzungumza kwa ufupi na wajumbe wa Tume hiyo ambayo iko chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhan.
Akizungumza na wajumbe wa Tume hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa ana uhakika kuwa wajumbe wa Tume hiyo watatimiza matarajio ya Watanzania katika kuifanya vizuri kazi ya Kukusanya na Kuratibu maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya.
“Nimefurahi kusikia kuwa mumeianza kazi yetu vizuri. Nawaombeni muwe huru kabisa katika kuifanya kazi yetu. Na kwa ubora wa sifa za wajumbe, binafsi, kama walivyo Watanzania wengine sina wasiwasi juu ya uwezo wenu kuifanya kazi hii vizuri,” Rais Kikwete amewaambia wajumbe waTume hiyo na kuongeza:
“Kilichobakia kwetu ni lini milango itafunguliwa ili tuanze kutoa maoni yetu …. huo ndiyo mchango wetu katika mchakato huu.”
Mapema akimkaribisha Mheshimiwa Rais, Jaji Warioba amesema kuwa Tume hiyo ilianza kazi kama ilivyotakiwa kisheria Mei Mosi mwaka huu na kuwa kazi ambazo zimefanyika mpaka sasa ni wajumbe kujielimisha kuhusu Sheria yenyewe ya Katiba na kuorodhesha Hadidu za Rejea za Tume.
“Mheshimiwa Rais tumetumia wiki hii ya kwanza ya kazi yetu kujielimisha kuhusu Sheria yenyewe iliyounda Tume hii na pia tumeorodhesha Hadidu za Rejea za Tume. Tumeanza pia maandalizi kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa umma na baada ya hapo tutatengeneza ratiba ya kazi yetu,” amesema Jaji Warioba na kuongeza:
“Tumeanza kuona kuwa kazi hii itakuwa siyo rahisi na muda ni mfupi lakini itafanyika. Tunakushukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ya uteuzi wa Tume na imani ambayo umeionyesha kwetu kwa kutuchagua kutumikia katika Tume hii.”
 
Rais pia amejulishwa kwa kazi ya kuajiri watumishi wa Tume hiyo imeanza na mpaka sasa wameajiriwa watumishi 29 kati ya 173 wanaotakiwa kufanya kazi kwenye tume hiyo ambayo itaifanya kazi ya Kukusanya na Kuratibu maoni kwa miezi 18 kuanzia Mei Mosi mwaka huu.

Halmashauri yagundua ubadhirifu dawa za mil.100/-

Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi imegundua udanganyifu na ubadhirifu mkubwa wa dawa unaofikia karibu Sh. milioni 100.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri ya Kilwa Adoh Mapunda, alifichua kuwa udanganyifu huo unafanywa na baadhi ya watumishi wa halmashauri wanaopokea dawa hizo kutoka Bohari ya Dawa (MSD ) na kuziingiza katika zahanati hewa ambazo hata ujenzi wake haujakamilika.
Ripoti hizo zinakuja wiki chache baada ya Bunge kuchachamaa kutaka ubadhirifu wa fedha na mali za umma ukomeshwe kwenye halmashauri na serikali kuu, hatua iliyosababisha baadhi ya Mawaziri kuwajibishwa wakiwemo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Mapunda , alikifahamisha kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika hivi karibuni juu ya ubadhirifu huo na kuongeza kuwa kwa miaka mitatu watumishi hao wameiba madawa yenye thamani ya Sh. milioni 83.2 kwa kuyaingiza kwenye zahanati hewa.
Alisema kiasi hicho cha dawa zilihujumiwa katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2010 kwa kusingizia kuwa kinapelekwa katika zahanati nane ambazo ujenzi wake haujakamilika.
Alizitaja zahanati hewa mbele ya baraza hilo kuwa ni Mitole, Hoteli Tatu, Kiranjeranje, Kisongo, Mchakama, Nangurukuru pamoja na vituo vya Mikole na Kimbalambala.
Kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi wa hesabu wa ndani iliyosomwa na mkurugenzi huyo alibainisha kuwa ukaguzi umeibua kuwepo vituo vinane ambavyo ujenzi wake haujakamilika lakini vimepatiwa usajili na kila kimoja hutengewa gawio la Sh milioni 7.3 kwa ajili ya dawa. Mkaguzi wa ndani alifanya uchunguzi wake katika vituo 51 vya kutolea huduma za matibabu.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa katika ukaguzi wa ndani ambaye yeye mwenyewe alimpatia jukumu la kufuatilia hujuma hizo mara baada ya kuhamishiwa kwenye halmashauri hiyo, imegundulika kuwa, vituo viwili kati ya hivyo vinane vilipewa gawio la dawa za thamani ya Sh.milioni 14.7 kila kimoja na vilivyosalia vilipata gawio la dawa za thamani ya Sh. milioni 7.3 kila kimoja.
Kutokana na takwimu zilizotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri inaonyesha kwamba madawa ambayo yalipelekwa kwenye zahanati hizo nane hewa yana thamani ya Sh. milioni 83.2 na haijafahamika mgao huo wa madawa ulikuwa ukipelekwa wapi.
Mapunda aliliambia baraza hilo la madiwani kuwa hali hiyo ni hujuma kubwa kwa serikali ambapo imeisababishia halmashauri kukumbwa na tatizo la kupelekewa dawa zisizohitajika, kwa maana kwamba kiasi hicho cha madawa kingeweza kupelekwa katika sehemu nyingine nchini.
Halmashauri ya wilaya ya Kilwa ina jumla ya zahanati 43, Vituo vya Afya vitano na hospitali mbili.
Baraza la madiwani ambalo lilimpongeza mkurugenzi huyo kwa kufanikisha kugundua ufisadi huo na lilipitisha azimio la kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, watumishi wote wanaotuhumiwa kufanya udanganyifu wa kupokea dawa kutoka Bohari ya Dawa na kuziingiza katika zahanati hewa.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wenzake, Mahadhi Nangoma, Diwani wa Lihimalyao, alisema hoja hizo zinapaswa kufanyiwa kazi ipasavyo ili iwe fundisho kwa watendaji wenye tabia ya kutumia vibaya madaraka yao.
Vitendo hivyo vya ubadhirifu vilifanyika wakati ambapo wakurugenzi zaidi ya wanne walikuwa wamefanyakazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kabla ya Mkurugenzi wa sasa kuhamishiwa katika halmashauri hiyo na kugundua ubadhirifu huo.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. KILWA FORUMS - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website
Proudly powered by Blogger